Slaa afufua ya EPA na rada, awabana Kikwete, Mkapa, DPP

Jamii Africa

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amefufua upya tuhuma za ufisadi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), huku akiwalaumu Rais Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuwa chanzo cha kutochukuliwa hatua mafisadi.

Dk. Slaa mbali ya kuwashutumu Kikwete na Mkapa, alielekeza shutuma pia kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Beno Ndulu, akisema kuwa chanzo kikubwa cha Watanzania wengi kuwa masikini wa kutupwa, huku mafisadi wakiachwa wakimiliki uchumi mkubwa na kujenga majumba nje ya nchi.

Dk Willibrod Slaa

Katibu Mkuu huyo wa Chadema ambaye alikua mgombea Urais wa chama hicho mwaka 2010,  ameshutumu vyombo vya dola na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Dk. Elieza Feleshi akivituhumu kwa kushindwa kumkamata na kumfikisha mahakamani, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Adrew Chenge, aliyehusishwa na tuhuma za rushwa iliyotokana na ununuzi wa rada nchini Uingereza hasa baada ya  kukutwa na mamilioni ya fedha katika benki za nje ya nchi.

Dk. Slaa ametoa kauli hiyo Jumapili Machi 17, 2012, alipozungumza kwenye kongamano la wanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), lililofanyika katika maeneo chuo hicho Nyegezi, Mwanza.

Akizungumza kwa kujiamini, Dk. Slaa amesema Rais Kikwete na Serikali yake ameshindwa kuwasaidia wananchi wake katika kudhibiti mifumuko ya bei, pamoja na kushuka kwa uchumi wa nchi.

“Kwa sasa nchi ipo pabaya sana, uchumi wa nchi umeshuka sana duniani. Ukiangalia Tanzania tulianza pamoja kiuchumi na nchi za Singapore na Malaysia….lakini kwa sasa nchi hizi zimetuacha mbali kiuchumi.
“Tanzania kwa sasa inashikilia nafasi ya tatu kwa umasikini duniani. Na ndiyo inayoongoza kwa wananchi wake kuwa masikini katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC). Tunataka mabadiliko, na mwaka 2015 Chadema imejipanga vema kushika dola,” alisema Dk. Slaa.

Alisema, Rais Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi ya Serikali yake ya kutoa fedha za kutosha kwa kila mwanafunzi na kwamba fedha nyingi zimekuwa zikiishia kwenye safari za Rais. Alisema hadi sasa amefikisha safari 325 tangu achaguliwe mwaka 2005.
Mbali na hayo, Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete kujitokeza hadharani kueleza fedha za EPA zilizopelekwa, kwani hakuna akaunti ya fedha hizo iliyofunguliwa na kuwekwa kwa fedha hizo, wala Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), na Bunge hawajui zilipo.

Rais Jakaya Kikwete

“Rais alilitangazia taifa kwamba mafisadi wa EPA wamerudisha fedha walizokwapua. Fedha hizi hakuna akaunti zilipofunguliwa, CAG hajui na hata Bunge na wabunge wake hawajui hizo fedha zipo wapi,” alihoji.
Katika hatua nyingine, aliishutumu Serikali ya Rais Kikwete kuwadanganya Watanzania juu ya mradi wa Kilimo Kwanza, akisema mradi huo umeasisiwa na watu fulani kwa maslahi yao, na alimuomba kiongozi huyo wa nchi ajitokeze aueleze umma iwapo Serikali yake ilikaa kuandaa mradi huo na nani waliokaa na tarehe gani.
Hata hivyo, alimtuhumu Rais Kikwete kutumia Baraza la Mawaziri kuligeuza kama sehemu ya ‘ulaji wa siasa’, kwani alisharuhusu Gavana BoT, Beno Ndulu kushiriki vikao vya Baraza hilo, wakati Gavana huyo haruhusiwi kuingia Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa sheria.
Alisema kinachofanyika hivi sasa ni danganya toto juu ya uchumi wa nchi, na kwamba takwimu zinazotolewa na benki Kuu hapa nchini si sahihi, alihoji kwamba: “Kama Gavana wa benki kuu anaingia kwenye baraza la mawaziri, anaenda kufanya nini kama si kupika takwimu za kiuchumi?. Takwimu za uchumi kukua kwa asilimia 6 zinatoka wapi?”.

Hata hivyo, alisema amekamata barua ya Rais Kikwete aliyoituma kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF), alilishukuru kwa kuisaidia Tanzania kifedha, na alisema hali hiyo inadhihirisha kwamba Tanzania ilivyoshamiri kwa kuombaomba.

Kuhusu Mkapa
.
Dk. Slaa alimtuhumu waziwazi Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kwa kile alichokiita kwamba kaharibu mfumo mzima wa uchumi wa nchi, kutokana na sera zake za ubinafsishaji ambapo baadaye alilazimika kujimilikisha mgodi wa mkaa ya mawe wa Kiwira.

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa

“Mkapa alibinsfsisha mashirika, makampuni na baadaye aliamua kujimilikisha  Kiwira. Huyu Mkapa ni mmoja wa viongozi walioiharibu sana nchi yetu hii,” alisema Katibu Mkuu huyo wa Chadema taifa.

Hata hivyo, alisema Rais huyo mstaafu pamoja na Rais Kikwete wamevunja rekodi duniani kwa kuruhusu makampuni ya kuchimba madini nchini kujenga viwanja vya ndege katika maeneo ya migodi kwa ajili ya kusafirisha madini, jambo alilosema kwamba ni kutoa njia ya kuruhusu kuibiwa kirahisi kwa madini.

“Tembea dunia nzima huwezi kuona nchi inayoruhusu mwekezaji kujenga viwanja vya ndege katika maeneo ya migodi yao. Kwa hapa Tanzania wenye migodi wameruhusiwa kujenga viwanja vya ndege ili wachukuwe kirahisi madini yetu na kuwaacha hoi Watanzania, hivi ni nchi gani hii?” alisema Dk. Slaa.

Gavana Ndulu

Slaa alisema Gavana wa Benki Kuu ameshindwa kuwashughulikia watu wanaotengeneza noti bandia, na kwamba

Dk. Benno Ndulu

Gavana huyo alishakabidhiwa mtuhumiwa na mashine ya kutengeneza noti bandia, lakini hadi sasa ameshindwa kulifanyia kazi suala hilo.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Gavana Ndulu na vyombo vya dola wakiwemo Makamanda wa Polisi nchini na Mkuu wa jeshi hilo (IGP), wameonekana dhahiri kuruhusu biashara ya kutengenezwa kwa noti bandia, hivyo kuharibu kabisa uchumi wa taifa.

Kuhusu Chenge
Dk. Slaa alihoji sababu ya Serikali ya CCM kushindwa kumkamata na kufikisha mahakamani, Andrew Chenge kwa tuhuma nzito zinazomkabili za ufisadi wa mamilioni ya fedha zilizokutwa katika akaunti huko nchini Uswisi.

“Chenge alikutwa anamiliki fedha nyingi sana huko nje ya nchi. Ushahidi ulishawasilishwa kwa DPP, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya Chenge,” alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa kwa nguvu zote.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

8 Comments
  • Hapa mzee umenenea,sio rahisi kwa uongozi huu kuwashitaki mafisadi kwa kuwa mafisadi ndo wanaowaweka madarakani viongozi wetu hivyo wanajikuta hawana nguvu ya kuwakama na kuwafungulia mashtaka.Hata Gavana hawezi kutumia taaluma yake kwa serikali hii tuliyonayo,yey ni sawa na rubber stamp anapangiwa cha kusema,kwa akili ya mtoto wa darasa la saba uchumi wa TZ kukua kwa 6% ni comedy….

    • kama slaa anao ushahidi si apeleke kwa vyombo vinavyohusika ili wenye tuhuma hizo wachukuliwe hatua kama alivyofanya Msemakweli aliyepeleka kwa DPP ushahidi wa Kagoda,si kuongea tu ktk kampeni haisaidii kitu kama kweli slaa anauchungu na nchi hii afanye hivyo na si kupiga kelele ktk majukwaa

      • Swala si kupeleka kwa DPP swala ni kupeleka kwa wananchi kwani unazungumzia Kigoda yupo wapi siyo waziri au nakosea

        Sauti ya umma ni wananchi waamue kusuka au kunyoa mwaka 2015 siyo mbali kama wananchi wataona kuna haja serikali ilyopo madarakani iondolewe kwa kura 2015 basi chama cha upinzani kitakachoshinda kinaweza kuwapeleka mahakamani.

        Hivyo nguvu kubwa ipo kwa wananchi wapiga kura
        Lakini yote tisa kubwa ni Amani yote yafanyike kwa amani

        Mungu ibariki Tanzania

  • taifa bado halijapata majibu muafaka kwa mada zote hizi,hivyo wajue wataendelea kuulizwa,hatujasahau na tunaamini miongoni mwa mambo yaliyochangia hali hii ngumu hayo ni miongoni mwao,ipo siku watajibu tu.

  • Mheshimiwa Dr.Slaa, mie binafsi nakushukutu sana kwa kujitolea mhanga kuwatetea Watanzania nikiwemo mimi. Hukujali kuhatarisha maisha yako! Hukujali kuchafuliwa jina, hukujali hata kukamatwa na vyombo vya dola na kuwekwa lockup! Yote hayo ni kwa ajili ya uchungu kwa ulonao kwa Watanzania wanaoteseka bila ya sababu yoyote! Mwenyezi MUNGU Akubariki sana Dr.Slaa.

  • Hivi hakuna taratibu za kisheria ambazo CHADEMA wanaweza kuzichukua kwa wanaowatuhumu kuliko kukalia kuongea kwenye majukwaa tu? Kama ushahidi upo ugumu uko wapi kwa CHADEMA au Dr. Slaa kuwafunguliwa watuhumiwa mashitaka na yeye akasimama kama mshitaki na mwananchi wa Tanzania?

    Mbona kwenye chaguzi imewezekana wananchi baki kuwafunguliwa mashitaka wabunge na wengine wamenyanganywa majimbo, kwanini isiwezekane kwenye hili la EPA? CHADEMA SIWAELEWI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *